Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

WHMTH YASIFIWA KWA MFUMO WA ANWANI ZA MAKAZI


 

Na Tagie Daisy Mwakawago

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari (WHMTH) ni miongoni mwa Wizara na taasisi nyingine za Kiserikali ambazo zimepongezwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri na ushirikiano katika kufanikisha Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022. 

Hafla rasmi ya kuzindua matokeo ya awali ya Sensa ya Taifa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 imehudhuriwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma tarehe 31 Oktoba 2022. WHMTH ilisimamia utekelezaji wa Operesheni Anwani za Makazi iliyofanyika kuanzia mwezi Februari 2022. Anwani za Makazi ni nyenzo muhimu iliyowezesha ukusanyaji wa takwimu za watu na makazi wakati wa Sensa.

Akizungumza jijini Dodoma, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na taasisi nyingine zilifanya Operesheni ya Anwani za Makazi vizuri kiasi kwamba ni sehemu ya mafanikio ya sensa ya mwaka huu 2022.

"Sasa nazindua matokeo yanayoonyesha kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina idadi ya watu milioni 61,741,120" alisema Rais Samia Suluhu Hassan. Idadi hiyo ni ongezeko kutoka idadi ya watu milioni 44.9 ya Sensa iliyofanyika mwaka 2012. 

Rais Samia alisema kati ya watu milioni  61.7, Tanzania Bara inachangia idadi ya watu milioni 59,851,357 wakati Zanzibar ina watu milioni 1,876,773. "Takwimu pia zinaonyesha kuwa katika milioni 61.7 wanawake ni milioni 31,687,990 ambayo ni sawa na asilimia 51; wakati idadi ya wanaume ni milioni 30,053,130 sawa na asilimia 49," anaeleza Rais.  Sensa ya Taifa ya mwaka 2022 ilifanyika kwa njia ya kidijiti, mfumo wa kisasa wa kukusanya takwimu ambao umepongezwa na jumuiya za kimataifa ikiwemo Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu Duniani (UNPF). 

Rais alizielekeza sekta zote kuhakikisha kuwa Mwongozo wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022-2030 unatekelezwa kwa kuzingatia mikakati ya kisekta, Ilani ya Chama Tawala ya mwaka 2020-2025 (Ilani ya  Chama Cha Mapinduzi), Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na mipango mingine ya maendeleo ya kimataifa izingatiwe ikiwemo Ajenda ya Umoja wa Mataifa ya Mwaka 2030 ya Maendeleo Endelevu.

Uzinduzi huo wa kihistoria ulishuhudiwa pia na Mh. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi; Mheshimiwa Kassim Majaliwa  Majaliwa  (Mb), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mhe. Hemed Suleiman Abdallah, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mama Anne Makinda, Kamishna wa Taifa wa Idadi ya Watu na Makazi; na Viongozi wengine Waandamizi wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Nape Moses Nnauye (Mb), Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari; Bi Rosemary Senyamule, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma na Dkt. Albina Chuwa, Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Tanzania.