Habari
MHANDISI KUNDO : USHIRIKIANO WA POSTA KENYA NA POSTA TANZANIA UTAONGEZA FURSA ZA AJIRA NCHINI
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb) ameeleza kuwa ushirikiano wa Biashara ya kuvuka mpaka "Cross border business" kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Kenya na uanzishwaji wa vituo maalum vya kubadilishana mizigo Kimataifa "Office of Exchange" utapunguza muda wa usambazaji na gharama za usafirishaji wa barua, vifurushi na Mizigo ya wateja pamoja na kuongeza fursa za Ajira.
Mhe. Kundo ameyasema hayo leo tarehe 01 Novemba, 2022 akimwakilisha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye aliyekuwa Mgeni Rasmi wa hafla ya Uzinduzi wa biashara ya kuvuka mpaka kati ya Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Kenya, kwenye mpaka wa Namanga Wilayani Longido.
"Gharama za usafirishaji na mizunguko mirefu ya vifurushi vya Wananchi kati ya Nchi hizi mbili unakwenda kupungua, lakini pia kutokana na kuanzishwa kwa vituo vya pamoja vya ubadilishanaji wa mizigo nimeona ziko fursa za ajira zinaenda kupatikana kwa watanzania" alizungumza Mhandisi Kundo.
Aidha Mhe. Kundo alieleza kuwa ushirikiano huu utaondoa usumbufu mkubwa uliokuwepo hapo awali, ambapo mteja anayetuma barua au kifurushi kutoka hapa Namanga, Arusha kwenda Nairobi, Kenya ilimlazimu kifurushi chake kurudi Dar es Salaam kwa ajili ya mchakato wa usafirishaji, kisha kitoke Dar es Salaam na kusafirishwa kwenda Nairobi, Kenya. Hivyo uwepo wa vituo hivi utapunguza mzunguko mrefu wa vifurushi vya wateja kwa kuwa mizigo itatoka Arusha moja kwa moja kwenda Nairobi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Kundo ametumia nafasi hiyo kulipongeza Shirika la Posta nchini kwa jitihada zake za kukuza mahusiano mazuri na Posta nyingine duniani huku akipongeza Shirika hilo kwa hatua kubwa ya ushirikiano huo wenye lengo la kurahisisha huduma za posta na usafirishaji.
Naye, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Ndugu Mohammed Abdulla amesema kuwa, Shirika la Posta ndio msingi wa Mawasiliano na Usafirishaji Nchini. Hivyo ushirikiano huu utazidi kuimarisha sekta ya usafirishaji na kurahisisha maisha ya wananchi.
Vilevile, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Ndugu Raymond Mangwala amelipongeza Shirika la Posta Tanzania na Shirika la Posta Kenya kwa ushirikiano huo wenye tija kwa wananchi na Taifa huku akilitaka Shirika la Posta kupanua wigo wa biashara mtandao.
Kwa upande wake, Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania Ndg. Macrice Mbodo ameeleza namna ambavyo Shirika hilo linavyoendelea kuboresha huduma zake za usafirishaji na Teknolojia ili kuwapunguzia wananchi adha ya kupata huduma za Posta pale wanapohitaji, huduma hizo mahali popote walipo. Aidha Postamasta Mkuu alimeongeza kuwa Shirika linaendelea na mageuzi ya kidijitalli ili kukuza ufanisi zaidi wa huduma zake.
Aidha, Uzinduzi huo ulihudhuriwa na Mwakalishi wa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia Kenya, Ndugu Paul Macharia, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Tanzania, Brigedia Jenerali Mstaafu Yohana Ocholla Mabongo na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika la Posta Kenya Ndugu Peter Kanaiya na Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Kenya ndugu Dan Kagwe.
Imetolewa na Kitengo Cha mawasiliano
Shirika la Posta Tanzania.