Habari
MAAGIZO YA RAIS SAMIA YATEKELEZWA
Na Georgina Misama – MAELEZO
Waziri wa Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Moses Nnauye (Mb) amekabidhi vifaa vya TEHAMA kwa jeshi la Polisi na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka leo Desemba 19, 2022 Jijini Dar es salaam, ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati ya hafla ya kukabidhi vifaa hvyo, Waziri Nape alisema Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ilipewa jukumu la kuhakikisha inaviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama kupata vifaa vya kisasa vinavyoendana na wakati ili kurahisisha utendaji kazi, ambapo alisema wataalam wamevikagua na kuhakikisha kuwa Vifaa vyote vinatolewa katika hafla hiyo vipo katika kiwango kizuri cha ubora na vitafaa kwa ajili ya madhumuni husika.
“Tunalo pia agizo la Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan la kuhakikisha tunaviwezesha vyombo vyote vinavyohusika na utoaji haki za watu ili haki ipatikane kwa wakati, urahisi na popote mtanzania alipo, sisi kama wizara husika wajibu wetu ni kuijenga Tanzania ya Kidijitali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha vyombo vinatimiza wajibu wao kwa kusaidiwa na TEHAMA aidha, tunamshukuru Mhe Rais kwa nia yake ya kuhakikisha watanzania wanakuwa salama na wanatimiza majukumu yao kama wanavyopaswa,” alisema Waziri Nape.
Katika hafla hiyo Waziri nape alikabidhi kwa Jeshi la Polisi kompyuta za “Desktop” mia moja na sabini (170), kompyuta mpakato (Laptop) kumi (10) na Modem za TTCL mia moja na sabini (170), ambapo kwa upande wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka walikabidhiwa Kompyuta mpakato (Laptop) mia moja na themanini (180), Scanner arobaini na tano (45) na Modem za TTCL thelathini (30).
Kwa upande wake Inspekta Jenerali Mkuu wa Jeshi la Polisi, Afande Camililius Wambura aliishukuru Serikali kwa kutambua umuhimu wa vifaa hivyo ambavyo vitaliwezesha jeshi la polisi kupokea mashtaka kutoka kwa wananchi kwa njia ya mtandao na kuwawezesha wananchi kufanya ufuatiliaji wa kesi zao popote walipo hivyo kurahisisha upatikanaji wa haki na taarifa kwa wakati.
“Jeshi la Polisi limejipanga kufanya kazi kwa vitendo zaidi, tunakwenda kutumia mfumo ambao utaonyesha hatua zote toka kupokelewa kwa kesi mpaka itakapofika mahakamani, vifaa hivi vitakwenda kufanya kazi hiyo kama ilivyokusudiwa, tumehangaikwa kwa muda mrefu kupata namna ambayo Jeshi litafanya kazi kisasa zaidi na kuepukana na mifumo ya kizamani, vifaa hivi vitatufanya tutimize malengo yetu,” alisema Afande Camilius.