Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

KUNDO ATOA WIKI MBILI UJENZI UKAMILIKE JENGO LA PAPU


Na Chedaiwe Msuya, WHMTH, ARUSHA.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo  Mathew amewaagiza wakandarasi wanaotekeleza mradi wa ujenzi wa jengo la Umoja wa Posta Afrika (PAPU) unaogharimu sh.bilioni 45 kukamilika ndani ya wiki mbili kwa ajili ya kuzinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kundo ameyasema hayo jijini Arusha katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa  jengo hilo ambapo amesema hadi kufikia Juni 20 liwe limekamilika na kuikabidhi serikali kwa ajili ya maandalizi ya ufunguzi huo.

"Nyie kama Wakandarasi tunahitaji muongeze nguvu na mfanye kazi usiku na mchana kutokana na muda wa kukabidhiwa umeshapita ambapo ilikuwa machi mwaka huu,"amesema

Amesisitiza kuwa ni vyema kazi hiyo ikafanyika kwa ubora  kwani kufanya hivyo ni moja ya kulitangaza Taifa pamoja na kujitangaza kibiashara  katika mataifa ya nje kwa kuacha alama ya jengo hilo

Muhandisi Kundo amesema ni vyema wakandarasi  wahakikishe kila kitu kiwe bora kifikie hadhi ya kimataifa kwani kwa kufanya hivyo ni moja ya kujitangaza kiutendaji kazi.

Aidha amesema kuwa Rais Samia kama kiongozi wa nchi anatekeleza  kazi zake katika kuhimarisha mahusiano na Mataifa mbalimbali hivyo ni vyema wakandarasi hao wasimuangushe katika utekelezaji wa mradi huo.

Kwa upande wake Mkandarasi Mshauri wa ujenzi wa jengo hilo, Bwn Christopher Sanga amesema maelekezo hayo yaliyotolewa na Naibu waziri yatafanyiwa kazi katika kuhakikisha wanakamilisha kwa wakati

Jengo hilo linatarajiwa kuzinduliwa mwezi Agosti, 2023 na Mhe. Dkt. Samia Suluhu  Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano..