Habari
KONGAMANO LA KUUNGANISHA WADAU WA TEHAMA LIMETOA MCHANGO MKUBWA KATIKA JITIHADA ZA SERIKALI YA TANZANIA NA MAPINDUZI YA ZANZIBAR KUKUA KIMAWASILIANO
Na Chedaiwe Msuya ,WHMTH, DAR ES SALAAM
Waziri wa miundombinu, mawasiliano na uchukuzi Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt Khalid Salum Mohammed amesema kongamano la kuunganisha wadau wa TEHAMA na Miundombinu (Connect 2 Connect Summit) lina mchango mkubwa katika ukuaji wa huduma za mawasiliano nchini kutokana na mchango wa kifikra na mawazo yaliyopatikana kwa siku zote mbili.
Waziri Khalid ameyasema hayo wakati akifunga kongamano hilo Septemba 8, 2022 na kueleza kuwa, Tanzania imepata wigo mkubwa wa kujua hatua zilizofikiwa na kila mmoja katika sekta ya mawasiliano ya kidigitali na kupata mbinu mbalimbali zitakazo saidia kukua kwa mawasiliano katika uchumi, afya na sekta zote nchini Tanzania na kuendana na kasi ya uchumi wa kidigitali.
“Sasa hivi tumeingia katika ulimwengu wa kidigitali na kila kitu kinakwenda katika hali hiyo na kasi sana na uchumi wetu pia tumeuegemeza huko na ukuaji wa huduma za mawasiliano tumewekeza huko, kwahiyo ni lazima na ni muhimu na sisi kama jamii katika dunia, kuwa sambamba na wenzetu wa digital age” amesema.
Amesema, katika kuhakikisha Tanzania ina imarika katika ulimwengu wa kidigitali, mwaka kesho kongamano hilo litafanyika upande wa Zanzibar kutokana na uwepo wa miundombinu rafiki inayowezesha Watanzania kunufaika kimawasiliano.
“Nchi yetu ipo tayari kwa kuwa na miundombinu ya kimawasiliano na yote ni kutonana na jitoihada kubwa zilizofanywa na serikali zetu mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nani kitu tumekiweka mbele katika ajenda ya maendeleo ya nchi yetu. Wao wamevutika na jitihada za serikali zetu zote mbili na mwakani tumeamua kufanya kwa upande wa Zanzibar” amesema.
Sambamba na hilo Waziri Khalid amefafanua kuwa, huduma za mawasiliano zimefikishwa nchi nzima katika mikoa na wilaya, ambapo zaidi ya asilimia 60 Tanzania bara, zimefikiwa na mkongo wa mawasiliano na upande wa Zanzibar wilaya zote 11 zimefikiwa pia.