Habari
JAMII ZA PEMBEZONI ZAENDELEA KUFIKIWA NA HUDUMA ZA MAWASILIANO
- Waziri Nape Aipongeza Kampuni Ya Tigo Kwa Kuanza Kukopesha Simu Janja
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Longido
Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa kushirikiana na kampuni za simu nchini imeendelea kufikisha huduma za Mawasiliano katika jamii za pembezoni.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye baada ya kuzindua mnara wa mawasiliano wa kampuni ya Tigo wenye teknolojia ya 2G na 3G uliojengwa kwa ruzuku kutoka UCSAF katika kata ya Noondoto wilaya ya Longido mkoani Arusha leo Machi 5, 2023.
Waziri Nnauye amesema Serikali ya Rais Samia inaendelea kuhakikisha kila mtanzania anafikiwa na huduma ya mawasiliano hasa jamii za pembezoni na maeneo yasiyo na mvuto wa biashara kwasababu mawasiliano yanachochea ukuaji wa uchumi, usalama na maendeleo ya mtu binafsi na nchi kwa ujumla.
Aidha, ametoa rai kwa wananchi hasa vijana kutumia huduma za mawasiliano kwa ajili ya maendeleo kwani zikitumika vibaya zinaweza kusababisha athari kwa jamii ikiwa ni pamoja na uharibifu wa maadili ya kitanzania.
Katika hatua nyingine Waziri Nnauye ameipongeza Kampuni ya simu ya Tigo kwa kuanza kukopesha simu janja kwa wananchi ikiwa ni hatua ya kuhakikisha wateja wao wanashiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijiti.
Inakumbukwa kuwa mwishoni mwa mwezi Januari, 2023 Waziri Nnauye alitoa rai kwa makampuni ya simu kuangalia uwezekano wa kuanza kukopesha simu janja kwa wananchi na kulipa kidogo kidogo wakati akizindua mnara wa mawasiliano mkoani Katavi.
"Tunajivunia utulivu wa kampuni ya Tigo na kuwafikia watanzania hadi vijijini na pia kwa kuanza kukopesha simu janja kwa wananchi kwa malipo ya shilingi 1000 kwa siku kwa mwaka mzima ili wananchi waanze kutumia huduma" ,amezungumza Waziri Nnauye
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Bw. Selestine Kakele amewataka wananchi wa jamii ya wafugaji katika kata ya Noondoto kutumia huduma za mawasiliano kutafuta fursa ya masoko ya mazao ya mifugo, kuongeza kasi ya shughuli za uchumi na kujiletea maendeleo.
Awali akitoa taarifa ya mradi huo, Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Bi. Justina Mashiba amesema Mfuko huo ni mfano wa ushirikiano baina ya Serikali na sekta binafsi (makampuni ya simu) ili kufikisha huduma za mawasiliano vijijini, maeneo ya pembezoni na yale yasiyokuwa na Mvuto wa Biashara.
"Katika mradi huu wa mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Noondoto UCSAF imetoa ruzuku ya shilingi milioni 104.9 kwa kampuni ya Tigo kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa mnara wa mawasiliano katika kijiji cha Noondoto",amefafanua Mashiba
Uzinduzi huo umeshuhudiwa na Mbunge wa Londido na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Dkt. Steven Kiruswa, viongozi wa Wilaya ya Longido pamoja na wafanyakazi wa Wizara hiyo, UCSAF na Kampuni ya simu ya Tigo.
I