Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

HUDUMA ZA MAWASILIANO NA TEHAMA KUSAIDIA KUKABILIANA NA MAJANGA


Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Dodomma

Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeandaa Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Mawasiliano wakati wa Majanga ili kusaidia katika kujiandaa, kugundua na kukabiliana na dharura na majanga ili kuzuia au kupunguza athari na maafa yanayoweza kutokea na kugharimu maisha, uharibifu wa rasilimali na miundombinu ya nchi.

Hayo yamebainishwa leo Februari 16, 2023 jijini Dodoma wakati wa mkutano uliowakutanisha  wadau mbalimbali kwa lengo la kutoa maoni yao kuhusu Mpango Mkakati huo.

Meneja wa Usimamizi wa Rasilimali za Mawasiliano na Teknolojia kutoka TCRA, Mhandisi Felician Mwesigwa,  amesema utekelezaji wa Mpango Mkakati huo utasaidia na kuwezesha upashanaji wa taarifa ndani ya Serikali, jamii iliyo hatarini, na kati ya mashirika ya umma na ya kibinafsi.

 Ameongeza kuwa malengo ya mpango  huo ni kuunganisha na kuboresha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha maeneo yote nchini yana uwezo wa kupokea tahadhari kupitia vyombo vyote vya mawasiliano kama vile simu za mkononi, redio, runinga na mitandao ya kijamii.

Kwa upande mwingine mpango huo umelenga kuhakikisha watoa huduma za dharura wanaweza kuwasiliana pindi mawasiliano ya msingi yameharibiwa, Urejeshwaji wa huduma za mawasiliano kwa haraka katika eneo lililoathiriwa na kuboresha ushirikiano wa kimataifa kwa kuridhia mikataba yenye kutoa msaada wa mawasiliano kwenye majanga.

Aidha, mpango mkakati huo umebainisha nambari maalum ya umma kuweza kutoa na kupokea taarifa kupitia kituo cha mawasiliano ya dharura kuhusu maafa yoyote yanayoendelea au kutokea nchini

Awali akifungua Mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Meja Jenerali Charles Mbuge amesema upo umuhimu wa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano na wadau wote wa masuala ya maafa nchini kwa lengo la kuhakikisha wanaendelea kuwa na mikakati madhubuti ya mawasilino wakati wa dharura.

 

.