Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

HOTUBA YA WAZIRI WA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI MHESHIMIWA NAPE MOSES NNAUYE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24


A. UTANGULIZI

Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa humu Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, ninaomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2022/23.

 

Aidha, ninaomba Bunge lako Tukufu lijadili na kupitisha Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

 

Naomba hotuba yangu yote iingie kwenye kumbukumbu za Bunge kama ilivyowasilishwa mezani.

 

Mheshimiwa Spika,

Awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha sote kuwepo hapa kushiriki katika Mkutano huu wa kumi na moja wa Bunge la kumi na mbili.

 

Mheshimiwa Spika,

Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uongozi wake madhubuti katika kipindi hiki cha zaidi ya miaka miwili ambacho kimekuwa na maendeleo na uwekezaji mkubwa katika Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

 

Kipekee nichukue nafasi hii kumshukuru sana Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Isdori Mpango kwa maelekezo yake na miongozo yake ambayo kwakweli imesaidia sana katika kutimiza majukumu yetu Wizarani.

 

Naomba pia kumshukuru sana Mhe Waziri Mkuu wa Tanzania Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa kwa usimamizi wake kwetu,miongozo yake na maelekezo yake kwetu ambayo yamekuwa chachu ya ufanyaji kazi wetu.

 

 

Wizara inatambua matarajio makubwa waliyonayo wananchi ya kufikishiwa huduma za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kama ilivyofafanuliwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020 - 2025.

 

Mheshimiwa Spika,

Nitumie fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza Bunge lako Tukufu kwa weledi, busara na hekima kubwa. Ninapenda kulishukuru Bunge lako Tukufu kwa ushirikiano wao wakati wote ninapotekeleza majukumu yangu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa mbalimbali kuhusu Wizara.

 

Mheshimiwa Spika,

Kwa upekee niishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu inayoongozwa na Mheshimiwa Seleman Moshi Kakoso Mbunge wa Jimbo la Mpanda Vijijini, Makamu Mwenyekiti Mheshimiwa Anne Kilango Malecela Mbunge wa Jimbo la Same Mashariki na Wajumbe wote wa Kamati.

 

Wizara imenufaika sana na umahiri, umakini na ushirikiano wa Kamati hiyo katika kuchambua, kushauri na kufuatilia majukumu yanayosimamiwa na Wizara. Ninapenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba maoni, ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati yamezingatiwa kikamilifu katika Hotuba hii. Nawaahidi mimi na wenzangu Wizarani, hatutawaangusha.

 

Mheshimiwa Spika,

Kwa masikitiko makubwa natoa pole kwako Mheshimiwa Spika na Wabunge wa Bunge lako Tukufu kwa kuondokewa na mpendwa wetu Hayati Mussa Hassan Mussa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Amani, Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi. Nitoe pole pia kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu, pamoja na wananchi wa Jimbo la Amani kwa kuondokewa na mpendwa wetu. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi, Amina.

 

Mheshimiwa Spika,

 

Wizara inasimamia Taasisi tisa, ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania; Shirika la Mawasiliano Tanzania; Shirika la Posta Tanzania; Shirika la Utangazaji Tanzania; Kampuni ya Magazeti ya Serikali; Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote; Tume ya TEHAMA; Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano na Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

 

 Hotuba hii itaelezea kwa ufupi masuala yanayotekelezwa na Wizara pamoja na Taasisi inazosimamia.

 

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara iliidhinishiwa kutumia kiasi cha Shilingi bilioni 282.06, Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 26.3 ziliidhinishwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na Shilingi bilioni 255.8 ziliidhinishwa kwa ajili ya Miradi ya Maendeleo.

 

Hata hivyo hadi kufikia mwezi Aprili, 2023 Wizara imepokea na kutumia jumla ya Shilingi bilioni 125.1. Kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 12.8 sawa na asilimia 48.7 ya fedha za matumizi ya kawaida na Shilingi bilioni 112.3 sawa na asilimia 43.9 ya fedha za mendeleo.

 

Ukusanyaji wa Mapato

Mheshimiwa Spika, kufikia tarehe 30 Aprili, 2023 Wizara imekusanya jumla ya Shilingi bilioni 24.9 kutokana na mauzo ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, tozo kuongeza salio, mauzo ya picha za Viongozi Wakuu wa nchi, machapisho na ada ya mwaka ya magazeti.

 

Aidha, Serikali kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania imeendelea na upangaji wa masafa kwa Huduma za Mawasiliano, ambapo mnada wa masafa ulifanyika tarehe 11 Oktoba, 2022 kwenye bendi za 700 MHz, 2300 MHz, 2600 MHz na 3500 MHz ambayo yanatumika kwa ajili ya mawasiliano ya simu na intaneti katika kuwezesha huduma za 4G na 5G nchini.

 

Makampuni manne ya ndani yalifanikiwa kushinda zabuni kwa mauzo ya Dola za Marekani milioni 187.5. Hadi mwezi Aprili, 2023 asilimia 75 ya fedha hizi kiasi cha Dola za Marekani milioni 140.6 zimeshalipwa na kuingia Mfuko Mkuu wa Serikali.

 

B. MAPITIO YA UTEKELEZAJI WA MPANGO NA BAJETI YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI NA TAASISI ZAKE KWA MWAKA WA FEDHA 2022/23

 

Katika Mwaka wa 2022/2023 Wizara imetekeleza masuala yafuatayo:-

 

Sekta ya Habari

 

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2022/23 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imefanya masuala yafuatayo:-

 

i.          Mapitio ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016 ambapo muswada wa marekebisho ya Sheria hiyo umesomwa Bungeni kwa mara ya kwanza mwezi Februari, 2023;

 

ii.         Imeratibu Mikutano 13 ya Msemaji Mkuu wa Serikali na kuainisha mafanikio ya Serikali na kutoa ufafanuzi wa masuala mbalimbali. Jumla ya Vipindi 25 vya Televisheni vinavyohusu utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo viliandaliwa na kurushwa hewani. Tumefanikiwa kujenga Studio ya muda Jijini Dodoma kwa ajili ya kuzalisha vipindi vya Kitaifa na kimkakati.

 

Pia, kumekuwepo na ongezeko la vituo 5 vya utangazaji wa maudhui ya ndani ya kulipia ambayo imetoa fursa ya ajira kwa wasanii wa ndani kwenye maudhui yenye muktadha wa filamu, michezo ya kuigiza na tamthilia.

 

TBC imeboresha maudhi yanayorushwa kwenye redio, televisheni na mitandao ya kijamii. Ubunifu wa kimaudhui na uwasilishaji umeongeza mvuto kwa vyombo vya Habari vya TBC. Aidha, TBC ilifanikiwa kununua HAKI za kutangaza michuano ya Kombe la FIFA la Dunia. Ambapo jumla ya michezo 28 (ilirushwa TBC ONE) na michezo yote 64 (ilirushwa TBC Taifa na TBC Online). Uanzishwaji wa kurusha taarifa ya Habari kwa Kiingereza umeanza mwezi Novemba, 2022 na hivyo kupanua wigo wa Habari zinazotolewa na Shirika hilo.

 

iii.        Vituo vya kurusha matangazo ya redio vimeongezeka kutoka 210 mwaka 2022 hadi kufikia vituo 215 Mwezi Aprili, 2023 na vituo vya kurusha matangazo ya runinga vimeongezeka kutoka 56 mwaka 2022 na kufikia vituo 65 Mwezi Aprili, 2023.

 

Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya matumizi ya teknolojia za Utangazaji hasa maudhui mtandaoni ambayo pia yamechangia kuongeza ajira kwa vijana. Katika kuimarisha usimamizi katika Sekta ya Habari Wizara kupitia TCRA na Idara ya Habari – Maelezo imetoa jumla ya leseni mpya 20 za magazeti zimetolewa na leseni 18 za maudhui ya mtandao zimetolewa;

 

iv.        Serikali imeendelea kuboresha huduma za Utangazaji hususani wa redio jamii katika maeneo ya vijijini. Serikali kupitia UCSAF imeendelea kujenga na kuboresha miundombinu ya kurushia matangazo na studio za redio ya Taifa katika maeneo ya kimkakati na mipakani. Maeneo mbalimbali Miradi hii imekamilika kama vile Mlimba Mkoani Morogoro, NgoroNgoro Mkoani Arusha, Ludewa Mkoani Njombe, Ruangwa Mkoani Lindi, Ngara Mkoani Kagera.

 

Mheshimiwa Spika,

v.         Kupitia magazeti ya Dily News, Habari Leo na Habari Mtandao Kampuni ya Magazeti ya Serikali Tanzania (TSN) imeendelea kutekeleza mpango wake mahsusi “Editorial Transformational Plan” kwa kuandika Habari za kina za uchambuzi.

 

vi.        Mradi wa kufunga mtambo mpya wa kisasa wa uchapaji unaendelea ambapo ununuzi na upokeaji wa mtambo wa magazeti  utafungwa;

 

Sekta ya Mawasiliano

 

Mheshimiwa Spika,

Kulingana na Kitabu cha Hali ya Uchumi wa Taifa, Sekta ya Habari na Mawasiliano imekua kwa kasi ya asilimia 9.1 mwaka 2020. Ukuaji huu unathibitishwa na ongezeko la upatikanaji na matumizi ya huduma za mawasiliano.

 

Mheshimiwa Spika,

Takwimu zinaonyesha laini za simu zilizosajiliwa kuongezeka kutoka milioni 55.7 Mwezi Aprili, 2022 hadi kufikia milioni 62.3 Mwezi Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 11.8.

 

Watumiaji wa intaneti wameongezeka kutoka Milioni 29.9 Mwezi Aprili, 2022 hadi kufikia Milioni 33.1 Mwezi Aprili, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 10.7. Takwimu hizi zinaashiria hali ya ukuaji wa Sekta.

 

Katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetekeleza majukumu yafuatayo:-

i.          Wizara inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003 ambapo rasimu imekamilika na kuwasilishwa kwa wadau;

 

ii.         Utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi na Kanuni zake ikiwemo mchakato wa uanzishwaji wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi.

 

iii.        Maboresho ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta kwa ajili ya kuweka mazingira wezeshi ambayo yamezingatia maslahi mapana ya wananchi pamoja na kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji;

 

iv.        Katika Sekta ya Mawasiliano tumefanikiwa kuandaa mkakati wa Sekta ya Mawasiliano wa kuimarisha ushiriki wa nchi Kikanda na Kimataifa ambapo Tanzania imefanikiwa kupata nafasi katika Baraza la Umoja wa Mawasiliano Afrika na Umoja wa Mawasiliano Duniani;

 

v.         Kufanikiwa kutekeleza Mfumo wa Anuani za Makazi Nchini kupitia Mradi wa Anuani za Makazi na Postikodi. Aidha, Mfumo wa Anuani za Makazi umeweza kuunganisha Taasisi za Umma kama vile Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuboresha taarifa za wamiliki wa viwanja, pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuboresha taarifa za walipa kodi.

 

vi.Usimamizi wa Huduma za Mawasiliano ya Simu na Intaneti ambapo jumla ya laini za simu 997 zilizokuwa zikitumika kwenye mawasiliano ya ulaghai wa mawasiliano ya simu za Kimataifa zilisitizwa matumizi yake;

 

vii.Usimamizi wa zoezi la usajili na uhakiki wa laini za simu Nchini ambapo hadi tarehe 30 Aprili, 2023 laini za simu zinazotumika kwenye Mitandao ya simu zimefikia milioni 63,317,168 zimesajiliwa kwa alama za vidole;

 

viii.      TCRA imetoa jumla ya leseni 26 kwa watoa huduma za Posta na Usafirishaji wa Vifurushi;

 

ix.        Ujenzi wa Jengo la Umoja wa Posta Afrika unaojengwa kwa ubia na TCRA ambapo utekelezaji wake umefikia asilimia 98

 

x.         Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limekabidhiwa rasmi jukumu la kutekeleza Mradi wa Mkongo wa Taifa (NICTBB), na Kituo cha Taifa cha Kutunzia Data (NIDC);

 

xi.        Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) limeendelea kufanya maboresho na usimamizi wa mifumo ya ukusanyaji kodi kwa njia ya kielektroniki ujulikanao kama e-RCS (Electronic Revenue Collection Sysytem);

 

xii.       Mikataba ya upelekaji huduma za mawasiliano vijijini imesainiwa ambapo jumla ya minara 758 kwa ajili ya kupeleka huduma za mawasiliano itajengwa na jumla ya Minara 304 itaongezewa nguvu chini hafla ambayo ilishuhudiwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Pia, jumla ya minara 42 katika Shehia 38 imekamilika na kuzinduliwa Zanzibar hafla ambayo ilishuhudiwa na Mheshimiwa Rais, wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri. Ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini ikiwemo maeneo ya Kimakati kama Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Julius Nyerere , Msomera- Handeni.

 

Eneo la TEHAMA

 

Mheshimiwa Spika;

Katika eneo hili Wizara imetekeleza yafuatayo;

i). Kusimamia na kuratibu utungwaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, ya mwaka 2022 Aidha, Wizara imekamilisha kuandaa Kanuni za kuwezesha utekelezaji wa Sheria hii;

ii). Kuwezesha kujenga uwezo wataalamu 500 wa Jeshi la Polisi kwenye nyanja ya usalama mtandao.

iii). Kusimamia maendeleo ya ujenzi wa  Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano

 

vi).Kukamilisha taratibu za kumpata Mshauri Elekezi wa kufanya upembuzi yakinifu wa Kituo cha Kuhifadhi Data Zanzibar

v). Kukamilisha upembuzi yakinifu wa kubaini maeneo yenye changamoto ya mawasiliano ili kuwezesha ujenzi wa minara 758 ambayo mikataba ya ujenzi wake imesainiwa tarehe 13 Mei, 2023 na kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

 

Mheshimiwa Spika,

Maeneo mengine ambayo Wizara imeendelea kuyafanyia kazi kwa kipaumbele ni pamoja na;

i). Ukamilishaji wa Mpango Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali (Digital Economy Framework 2023-2033),

ii). Kuhuisha ununuzi wa Mkondo wa Mawasiliano ya Serikali (Extension of Government Internet Bandwidth) wenye kasi ya 5Gbps,

iii). Kufanikiwa kuandaa Daftari la huduma za Serikali kwa ajili ya kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi (Government Service Directory) ambapo taarifa zimekusanywa kutoka Taasisi 57 za Serikali.

iv). Kuendelea na utekelezaji wa mradi wa kuendeleza Ubunifu na Utengenezaji wa Vifaa vya TEHAMA, ambapo shughuli zifuatazo zimetekelezwa: kukamilika kwa usanifu wa Kituo cha Kampuni changa za TEHAMA cha Kanda ya Dar es Salaam na kutengeneza mfumo jumuishi utakaowezesha kuwa na taarifa za wabunifu, kampuni za TEHAMA, wawekezaji katika huduma na bidhaa za ubunifu katika TEHAMA, Vituo atamizi vya TEHAMA na Vituo vya uendelezaji bunifu za kidijitali.

 

Mheshimiwa Spika,

Utekelezaji wa Majukumu ya Taasisi zilizo chini ya Wizara umeainishwa katika Ukurasa wa 34 hadi 59 wa Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

 

 

C. MPANGO NA MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA FEDHA KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24

 

Makadirio ya Mapato ya Wizara

 

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Wizara inakadiria kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 150.7 ambazo zitatokana na mauzo ya huduma za;

i). Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano,

ii). Tozo itokanayo na kuongeza salio la simu,

iii). Usajili wa Magazeti na ada ya mwaka ya Magazeti,

iv). Vitambulisho vya Waandishi wa Habari na machapisho ya picha, mabango na majarida.

 

MALENGO YA BAJETI YA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KWA MWAKA FEDHA 2023/2024

 

Eneo la Habari

 

Mheshimiwa Spika,

Katika Sekta ya  Habari Wizara itatekeleza majukumu yafuatayo:

(i)        Kufanya mapitio ya Sera ya Habari na Utangazaji ya Mwaka,2003 ilikuendana na mabadiliko katika Sekta ya Habari,

(ii)        Kuratibu utungwaji wa Sheria ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC),

(iii)       Kujenga studio maalum kwa ajili ya vipindi vya moja kwa moja vya redio na televisheni,

(iv)      Kuanzisha redio ya Afrika itakayotangaza kwa lugha ya kiswahili kwa lengo la kuendeleza matumizi ya kiswahili na kujenga umoja wa Afrika.

(v)       Kuendelea kusimamia Sekta ya Habari kwa kutoa Leseni

(vi)      Kuhamasisha vyombo vya habari vya nje katika kutangaza Tanzania

(vii)      Kuendelea kujenga na kufunga miundombinu ya utangazaji katika Wilaya tisa kati ya Wilaya 21 ambazo hazina usikivu au zina usikivu hafifu;

(viii)     Kuendelea na ujenzi wa Makao Makuu ya TBC Jijini Dodoma;

(ix)      Ununuzi wa mitambo na vifaa vya utangazaji vya redio, Televisheni na Mitandao ya kijamii kwa lengo la kuunganisha studio tano za Mikocheni, Zanzibar, Barabara ya Nyerere, Dodoma na Arusha,

(x)       Kununua gari moja ya kurushia matangazo ya Televisheni mbashara,

(xi)      Kukamilisha ujenzi wa majengo ya kiwanda cha uchapaji na kufunga mitambo ya kisasa ya uchapaji,

(xii)      Kuanza taratibu za ujenzi wa Kituo cha Habari ambacho kitajumuisha Chaneli ya Televisheni ya Serikali, studio ya kuzalisha maudhui, vyumba vya mikutano, mifumo ya kufuatilia habari zinazotokea duniani na kutoa fursa kwa waandishi wa habari kufanya kazi pamoja.

 

Eneo la Mawasiliano

 

Mheshimiwa Spika,

Wizara imepanga kutekeleza majukumu yafuatayo: -

i.          Kufanya mapitio ya Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya Simu ya Mwaka 1997 na kukamilisha uhuishaji wa Sera ya Taifa ya Posta ya Mwaka 2003;

ii.         Kuratibu uimarishaji wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya simu na Posta kote nchini

iii. Kuanzisha utaratibu mahususi wa kugawa masafa kwa ajili ya redio za utangazaji kidijitali;

iv.Kuratibu utungwaji wa Sheria ya kuimarisha matumizi na kuhakikisha uendelevu wa mfumo wa Anwani za Makazi;

v.         Kuratibu uanzishwaji wa anga la Juu nchini ikiwemo kufanya maandalizi ya kurusha Satelite katika kuwezesha urahisi na unaafuu katika upatikanaji wa huduma za Mawasiliano Nchini.

vi.        Kuandaa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya Mawasiliano,

vii.       Kusimamia utekelezaji wa biashara Mtandao (e-Commerce).

viii.      kuratibu uanzishwaji wa maghala maalum ya kuhifadhi bidhaa, huduma ya ugomboaji na ushuru wa forodha ili kuwezesha biashara mtandao

ix.        Kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Brodibandi wenye kasi zaidi (National Broadband Strategy);

x.         Kuratibu utekelezaji wa mradi wa miundombinu ya mawasiliano ya simu, redio na televisheni vijijini.

xi). Ukamilishaji wa shughuli za ujenzi wa Kilometa 1,742 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa Kuratibu ujenzi wa Kilomita 60 za mkongo wa mawasiliano kupitia Ziwa Tanganyika kuunganisha Tanzania na Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo, Kuratibu ujenzi wa Kilometa mpya 1,600 za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na kufikisha huduma ya Mkongo kwenye Wilaya 14,na Kujenga Mikongo ya kuunganisha watumiaji ambao ni Taasisi 50 kwenye maeneo ya uwekezaji, huduma za afya na elimu ili kuharakisha Taifa kushiriki katika uchumi wa kidijitali.

 

Eneo la TEHAMA

 

Mheshimiwa Spika,

Katika kuimarisha matumizi ya TEHAMA nchini, Wizara inatarajia kutekeleza majukumu yafuatayo: -

i.          Kuhuisha Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016 na kuandaa Mkakati wa utekelezaji,

ii). Kuandaa Mkakati wa Kitaifa wa matumizi ya Teknolojia zinazoibukia(emerging technologies) kama vile Artificial Intelligence,   Robotics,                  IoT, ili kuiwezesha nchi kufikia Mapinduzi ya Nne ya viwanda(4th Industrial Revolution)

ii.         Kuratibu na kuwezesha matumizi ya Mfumo wa Mikutano ya Video (video conferencing) katika ngazi ya Wizara, Mikoa 26 na Halmashauri 185 nchini;

iii.        Kufanya tathmini ya uanzishwaji wa ‘smart cities’ katika mikoa ya Dodoma, Arusha na Mbeya;

iv.Kuendelea na uratibu wa uendelezaji wa Mifumo ya Kitaifa nchini;

v.         Kuandaa Mkakati wa kuboresha matumizi ya Tafiti za TEHAMA,

vi.        Kuendelea kuboresha Usimamizi na uanzishwaji wa Kampuni Changa za TEHAMA kwa kuboresha mazingira ya Kisera, Kisheria na Kikanuni na kuweka miongozo stahiki.

vii.       Kuanzisha vituo vitano vya kanda vya kusaidia kukuza Taaluma na ubunifu wa TEHAMA;

viii.      Kuunganisha Taasisi za Serikali kwenye mtandao mmoja (GoVNET);

ix.        Kuwezesha usimikaji wa Vituo vya Huduma Pamoja nchini;

x.         Kujenga maabara tatu kwa ajili ya kufufua vifaa vya TEHAMA katika Mikoa ya Arusha, Dar es Salaam na Mwanza; na

xi.        Kujenga uwezo kwa wataalam wa TEHAMA 500 Serikalini katika maeneo yenye wataalamu haba ikiwemo Artificial Intelligence,Big Data Analytics,Machine Learning, Augumented Reality.

xii. Ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Kuhifadhi Data Zanzibar na kufanya upembuzi yakinifu kwa ajili ya uanzishwaji wa Kituo cha Taifa cha Data Dodoma; pamoja na kusimamia uanzishwaji wa Vyuo viwili vya TEHAMA vya Nala na Kigoma,

 

Mheshimiwa Spika,

 

Serikali ya Awamu ya sita imedhamiria kuwezesha nchi kuelekea katika uchumi wa kidijitali hususani kuhimiza mfumo wa kufanya biashara bila fedha taslimu (cashless economy) ambao unaowezeshwa na kuendeshwa na TEHAMA.

 

Ili kufanikisha haya kwenye Sekta zote za Uchumi na Kijamii, Wizara imepanga kufanya mabadiliko na maboresho makubwa kwenye Sekta ili kuendana na mageuzi haya ikiwemo kuharakisha ujenzi, uendelezaji na usimamiaji miundombinu ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

 

Vilevile, Wizara itafanya mapinduzi kwenye Taasisi za Sekta kwa lengo la  kuimarisha mashirikiano na Sekta binafsi, kuendeleza tafiti na ubunifu kwenye masuala ya TEHAMA ikiwemo uanzishwaji na uendelezaji wa kampuni changa (startups), kuwezesha Sekta nyingine kuelekea kwenye mapinduzi haya ya kidijitali; na kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari nchini.

 

Aidha, Wizara yangu itahakikisha Uchumi wa Kidijitali unawekewa mazingira bora ya kiudhibiti na kiuwekezaji ikiwemo kuandaa sera, miongozo na taratibu za kulinda maadili ya Kitanzania na kuhakikisha usalama mtandaoni.

 

Eneo la Usalama Mtandao

 

Mheshimiwa Spika,

Wizara inatarajia kutekeleza majukumu yafuatayo:-

(i)        Kufanya tathmini ya Mkakati wa Kitaifa wa Usalama Mtandaoni 2018 - 2023 na kuandaa na kutekeleza Mkakati mpya wa 2023 - 2028;

(ii)        Kusimamia utekelezaji wa Mkakati wa Elimu kwa Umma kuhusu Usalama Mtandao 2021/22 - 2025/26;

(iii)       Kusimamia ukamilishwaji na utekelezaji wa usimamizi wa Miundombinu Muhimu ya TEHAMA (Critical ICT Infrastructures);

(iv)      Kuimarisha muundo wa kiutawala na kiusimamizi wa ulinzi dhidi ya uhalifu wa mtandao nchini; na

(v)       Kuimarisha uwezo wa wakaguzi wa ndani kufanya ukaguzi wa mifumo.

 

Mheshimiwa Spika,

Ili kujenga uwezo wa Wizara kuendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi. Shughuli zifuatazo zitatekelezwa:-

i)          Kuendeleza watalaam wa ndani na nje ya Sekta kwa kutoa mafunzo ya usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya TEHAMA na elimu ya matumizi ya teknolojia mpya zinazoibukia kwenye sekta nyinginezo;

ii)         Kuwajengea uwezo Waandishi wa Habari na Wahariri wa Vyombo vya Habari;

iii)        Kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa kununua vitendea kazi; na

iv)        Kuelimisha umma juu ya teknolojia mpya za kidijitali, kwa kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama na yenye tija ya TEHAMA huku wakilinda haki za watoto, wanawake, makundi maalum na vijana.

 

Mheshimiwa Spika,

Shughuli zitakazotekelezwa na Taasisi tisa zinazosimamiwa na Wizara zimeainishwa kwenye ukurasa Na. 74 hadi 82 wa Kitabu cha Hotuba ya Bajeti.

 

SHUKRANI

 

Mheshimiwa Spika,

Kwa moyo wa dhati ninapenda kuwashukuru wale wote walioshiriki kunisaidia kutekeleza majukumu yangu katika Wizara hii. Kipekee niwashukuru Mheshimiwa Mhandisi Kundo Andrea Mathew (Mb.), Naibu Waziri; Mohammed Khamis Abdulla, Katibu Mkuu na Selestine Gervas Kakele, Naibu Katibu Mkuu.

 

Aidha, naishukuru Menejimenti ya Wizara, Wenyeviti wa Bodi za Wakurugenzi za Taasisi zinazosimamiwa na Wizara; Viongozi wa Taasisi na wafanyakazi wote wa Wizara na Taasisi kwa kufanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa Wizara yetu inakuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

 

Mheshimiwa Spika,

Naomba kipekee nichukue fursa hii kuwashukuru Washirika wa Maendeleo ambao Serikali imekuwa ikishirikiana nao katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo katika Sekta za Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.

 

Baadhi ya washirika hao ni: Shirika la Umoja wa Mataifa la Mawasiliano; Shirika la Umoja wa Posta Duniani; Shirika la Umoja wa Posta Afrika; Benki ya Dunia kupitia dirisha la Wakala wa Maendeleo ya Kimataifa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa.

 

Mheshimiwa Spika,

Ningependa pia kuzishukuru Jumuiya za Kikanda na Kimataifa za Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na Jumuiya ya Ulaya kwa ushirikiano katika masuala ya Kikanda na Kimataifa yanayohusu Sekta hii. Kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2023/24, Wizara yangu itaendelea kuimarisha ushirikiano na Washirika wa Maendeleo na wadau wengine ili kuhakikisha kuwa Sekta ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inachangia katika kutimiza Dira ya Taifa ya kufikia Uchumi wa Kati wa Juu ifikapo Mwaka 2025.

 

Mwisho sio kwa umuhimu naomba kuwashukuru kwa dhati wananchi wenzangu wa Jimbo la Mtama kuendelea kuniamini na wakati mwingine kunivumilia wakati natimiza majukumu yangu. Nina wapenda na kuwathamini sana, tuendelee kuchapa kazi pamoja.

 

Siwezi sahau upendo, uvumilivu na kunitia moyo kwa familia yangu wakiongozwa na binti yangu Jayla, wanangu Jaydan na Jayson na mama yao mke wangu Rhobi. Nawashukuru kwa upendo wao, kunivumilia hasa ninapokosekana kwa muda na namna wanavyonitia moyo katika kutimiza kazi zangu.

 

MUHTASARI WA MAOMBI YA FEDHA KWA WIZARA YA HABARI, MAWASILIANO NA TEKNOLOJIA YA HABARI KWA MWAKA WA FEDHA 2023/24

 

Mheshimiwa Spika,

Katika Mwaka wa Fedha 2023/24, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inaomba kuidhinishiwa jumla ya Shilingi 212,457,625,000 kwa mchanganuo ufuatao:-

i)          Kiasi cha Shilingi 30,503,685,000 kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Shilingi 18,522,155,000 ni za Mishahara na Shilingi 11,981,530,000 ni za Matumizi Mengineyo; na

 

ii)         Kiasi cha Shilingi 181,953,940,000 kwa ajili ya utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo ambapo Shilingi 146,777,440,000 ni Fedha za Ndani na Shilingi 35,176,500,000 ni Fedha za Nje.

 

Mheshimiwa Spika,

Hotuba hii inapatikana katika tovuti ya Wizara ambayo ni http://www.mawasiliano.go.tz na pia kwa kutumia QR Code ambayo imesambazwa kwenu.

 

Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.