Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. YONAZI AKAGUA UJENZI WA MIUNDOMBINU YA TEHAMA YA KILOMITA 265


Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Jim Yonazi akikagua kituo cha maunganisho ya Mkongo wa Mawasiliano wa Taifa wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya mkongo huo kutoka Manyoni, Singida mpaka Kambikatoto mkoani Mbeya.

 

Prisca Ulomi na Daudi Manongi, Kambikatoto- Singida

Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi amefanya ziara ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya TEHAMA yenye urefu wa kilomita 265 ambao umefanyika kwenye eneo la Itigi, Manyoni mkoani Singida hadi eneo la Kambikatoto, Mbeya. Ukaguzi wa ujenzi wa miundombinu hiyo ni pamoja na ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa kilomita 265, vituo vya kutolea huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano na vituo vya kuongeza nguvu za mawasiliano.

Dkt. Yonazi amesema kuwa amefanya ziara hiyo ili kukagua ujenzi huo kwa lengo la kujiridhisha na maendeleo ya ujenzi huo ili kuona namna mkandarasi ametekeleza kazi husika kwa kuwa Serikali imetoa shilingi bilioni nane za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo iliyojengwa eneo la Itigi, Manyoni hadi Kambikatoto

Ameongeza kuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za mawasiliano, za uhakika na kwa gharama nafuu katika maeneo yote nchini nzima ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanaendelea kutumika katika shughuli za kiuchumi na kijamii katika kuchochea maendeleo ya taifa letu

Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa miundombinu hiyo, Rajab Mikumwo wa Kampuni ya  Raddy Fibre Solutions ambaye ni mkandarasi aliyejenga miundombinu hiyo amemweleza Dkt. Yonazi kuwa, kampuni yao imetekeleza ujenzi wa miundombinu hiyo kwa mujibu wa matakwa ya mkataba na tayari nyaya za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano zimelazwa ardhini na katika baadhi ya maeneo nyaya hizo zimepitishwa juu ya nguzo kuendana na jiografia ya eneo husika endapo kuna mto au mwamba ili kuhakikisha kuwa mawasiliano yanapatikana kwa uhakika mwanzo hadi mwisho wa eneo husika

Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa tayari Serikali imefikisha miundombinu hiyo kwenye maeneo ya mipaka ya nchi za jirani zinazopakana na Tanzania na sasa hatua zinaendelea za kufikisha mawasiliano hayo mpakani mwa DRC Congo na Tanzania ili nchi jirani ziendelee kutumia na kunufaika na miundombinu hiyo

Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Miundombinu ya TEHAMA wa Wizara hiyo, Mhandisi Nikusubila Maiko amesema kuwa ujenzi wa miundombinu hiyo utawezesha watoa huduma za mawasiliano nchini kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi kwa kuwa tayari watoa huduma hao wamewasilisha mahitaji hayo Wizarani ambapo ujenzi wa miundombinu hiyo utaongeza kasi ya matumizi ya TEHAMA kwa taasisi za Serikali, sekta binafsi na wananchi walio kwenye maeneo hayo ambapo miundombinu hiyo imejengwa.