Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. NDUGULILE AKAGUA MAANDALIZI YA UZINDUZI WA HUDUMA PAMOJA


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya ziara yake ya kukagua maandalizi ya uzinduzi wa Huduma Pamoja katika Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania, Dar es salaam. Kushoto kwake ni Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano Wizarani, Mhandisi Clarence Ichwekeleza. Kulia ni Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Macrice Mbodo.

Dar es Salaam

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile, amekagua maandalizi ya uzinduzi wa Huduma Pamoja utakaofanyika Septemba 6 mwaka huu katika viwanja vya Makao Makuu ya Shirika la Posta Tanzania Jijini Dar es Salaam na kuarifu umma kuwa Mgeni rasmi wa uzinduzi huo ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa

Katika ukaguzi huo Dkt. Ndugulile amesema mikakati iliyoko kwasasa ni kulifanya Shirika hilo kuwa kitovu cha Biashara Mtandao ambapo  katika juhudi ya kulifanikisha hili, Serikali tayari imewekeza shilingi bilioni 3.9 kati ya shilingi bilioni 7.8 ilizoahidi kulipatia Shirika hilo.  Fedha hizo zitatumika katika mabadiliko ya kidijitali ndani ya Shirika, pamoja na ununuzi wa vitendea kazi vya usafirishaji, kama vile pikipiki, bajaji na magari. 

Aidha Dkt, Ndugulile ameeleza ukuaji wa teknolojia unaoendelea kufanyika ndani ya Shirika hilo kwa kuainisha huduma mbalimbali za kidijitali ikiwemo Duka mtandao la Posta "Posta Online shop" pamoja na Posta kiganjani, huku akiahidi Serikali kulinda watumiaji wa mtandao na kupambana na matapeli wa mitandaoni ili kurahisisha ukuaji wa biashara hizi za mtandao nchini. 

Dkt. Ndugulile aligusia mradi  wa dola milioni 150 za kimarekani za Mradi wa Tanzania ya Kidijitali ambapo kati ya hizo dola milioni 21.5 za kimarekani ambazo ni sawa na shilingi bilioni 49.8 zitatumika kwenye vituo vya Huduma Pamoja nchini.

Aidha, aliongeza kuwa Tanzania imepata ushindi kwa kuwa Mjumbe wa Baraza la Utawala na Baraza la Uendeshaji la Umoja wa Posta Duniani ambao aliainisha faida zitakazopatikana kwa ushindi huo ikiwemo ya Tanzania kupata nafasi ya kuwa sehemu ya watoa maamuzi ya mambo mbalimbali yanaogusa moja kwa moja Sekta ya Posta nchini, Afrika kwa ujumla na ndani ya Umoja huo katika ngazi ya dunia. 

Kwa upande wake Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, alieleza namna ya kujisajili na duka mtandao wa Shirika hilo na faida ambazo Shirika pamoja na mteja anapata katika duka hilo. 

“Mfanyabiashara anapojiunga katika huduma ya duka mtandao na kuuza bidhaa zake sisi kama Shirika la Posta tunapata asilimia 3 ya bei ya bidhaa sambamba na gharama za usafirishaji na hilo limepelekea Shirika kupata milion 300 toka kuzinduliwa kwa huduma ya duka mtandao,” amesema Mbodo. 

Mbodo alieleza uelekeo wa Shirika hilo katika kuziweka huduma zake zote kiganjani ambapo namba ya simu ya mteja itakuwa anwani yake. Aliongeza kuwa kwa awamu ya kwanza kutakuwa na vituo kumi vya Huduma Pamoja kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza, Arusha, Kigoma, Mbeya, Tanga, Morogoro, Kigoma, Mjini Magaribi-Unguja na Chakechake Pemba na awamu ya pili itakuwa mikoa 17 hivyo kufikisha huduma hiyo nchi nzima.

Shirika la Posta linazindua rasmi huduma ambayo itazikutanisha Taasisi mbalimbali za Serikali na kutoa huduma kwa pamoja ikiwemo BRELA, NIDA, NSSF, RITA, TRA Uhamiaji, PSSF, NHIF na nyinginezo ambazo zitatoa huduma kwa pamoja kupitia ofisi za Posta nchini.