Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. KIJAJI AIKUMBUSHA MENEJIMENTI YA WIZARA YAKE KUTEKELEZA WAJIBU


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na Menejimenti ya Wizara hiyo Mji wa Serikali Mtumba mara baada ya kuapishwa Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma. Kulia ni Naibu Waziri wake, Mhandisi Kundo Mathew na  kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula

 

Prisca Ulomi na Faraja Mpina, DODOMA

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Dkt. Ashatu kijaji ameitaka Menejimenti na watumishi wa Wizara yake itambue kuwa lengo na dhumuni la kuundwa kwa Wizara hiyo ni kuwatumikia wananchi kwa kutekeleza kile kilichoelekezwa kwenye Ilani ya CCM ya 2020-2025 kwa kuzisoma na kuziishi kurasa zinazohusu Wizara hiyo

Hayo ameyazungumza Dkt. Kijaji katika kikao chake cha kwanza na Menejimenti ya Wizara hiyo kilichofanyika katika ofisi za Wizara zilizopo Mtumba mara baada ya kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Ikulu ya Chamwino, Dodoma

Dkt. Kijaji amesema kuwa watendaji wa Wizara hiyo wanatakiwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi mkubwa kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kwa sababu umma wa watanzania una uchu wa kusikia kinachoendelea duniani hivyo kabla ya kufungia chombo chochote cha habari ni vema kutekeleza wajibu kwanza

“Mifumo yote ya Taifa hili ipo chini ya Wizara hii na tumeunganishwa na Sekta ya Habari, twendeni tukahakikishe tunafanya kazi kwa matokeo yanayoonekana”, amesema Dkt. Kijaji

Amesema kuwa matarajio yake ni kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na upendo baina ya viongozi wa Wizara hiyo bila kusuguana kwa kufuata utaratibu wa utumishi wa umma ikiwemo kutunza siri za Serikali na kutoa taarifa sahihi kwa umma

Kwa upande wa Naibu Waziri wa Wizara hiyo Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa maelekezo aliyoyatoa Waziri wake yamelenga kufanya kazi kwa matokeo yanayohitajika ili baadae yaoneshe mabadiliko katika jamii wanayoitumikia na kuahidi kuwa yeye binafsi pamoja na Menejimenti nzima ya Wizara hiyo imepokea maelekezo hayo na inaenda kuyafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa

 Awali Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula aliitambulisha Menejimenti ya Wizara hiyo akiwemo Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO baada ya Sekta ya Habari kumegwa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na kuhamishiwa kwa iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na kuunda Wizara mpya Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Dkt. Chaula amesisitiza menejimenti hiyo kuendelea kufanya kazi kwa kufuata Sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma ili matokeo ya kazi na majukumu ya kila mmoja wao iwe yenye tija na ufanisi mkubwa

Naye Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari, MAELEZO, Gerson Msigwa kwa niaba ya Menejimenti hiyo amesema kuwa wamepokea maelekezo ya Waziri huyo na kuahidi kuwa watii, wasikivu na kuchapa kazi kwa kiwango ambacho kimetolewa muongozo na kiongozi huyo