Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. CHAULA: SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA SEKTA BINAFSI KUKUZA MATUMIZI YA TEHAMA NCHINI


 

 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika Sekta ya afya na elimu nchini.

 

Dkt Chaula ameyazungumza hayo alipokuwa akifungua kikao cha wadau cha kujadili mkakati wa kukuza na kuendeleza matumizi ya TEHAMA katika vituo vya afya na shule nchini kilichofanyika katika katika ukumbi wa mikutano wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma

 

“Serikali inatambua mchango wa Sekta binafsi pamoja na washirika wa maendeleo katika jitihada za kuboresha matumizi ya mifumo ya TEHAMA nchini, kuna haja ya wadau kushirikiana na Serikali ili kuwa na uratibu mahsusi wa kukuza matumizi ya TEHAMA pamoja na maendeleo yake hasa katika eneo hili la elimu na afya”, Dkt. Chaula

 

Amesema kuwa kutokana na mabadiliko na muingiliano wa teknolojia duniani huduma nyingi zimekuwa zikitolewa kupitia TEHAMA kitu kilichopelekea Serikali kupitia Wizara hiyo kuhakikisha kuwa huduma zinazotolewa na kila mmoja kwa wakati wake zinaenda sambamba na Sera ya Taifa ya TEHAMA ya mwaka 2016.

 

Aidha, Dkt. Chaula amesema Serikali imejenga na kusambaza Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambao ndio njia kuu ya upatikanaji wa huduma mawasiliano ya simu na intaneti nchini ili wananchi na taasisi zote za umma ziweze kupata huduma za mawasiliano ya uhakika kwa gharama nafuu.

 

Naye Mkurugenzi wa Kiufundi wa Mifumo kutoka katika Shirika linalojihusisha na kuimarisha mifumo ya Sekta ya umma (PS3+) Desderi Wengaa amesema kuwa Shirika hilo lipo tayari kushirikiana na Wizara hiyo kwa kutoa usaidizi wa wataalamu wa kiufundi pamoja na fedha ili kuwezesha utekelezaji wa Mkakati wa pamoja wa matumizi ya TEHAMA katika vituo vya elimu na afya nchini.

 

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Idara ya TEHAMA wa Wizara hiyo Mulembwa Munaku amesema kuwa lengo la mkakati huo ni kuweka utaratibu mahsusi utakaoratibiwa na Wizara hiyo wa upelekaji wa huduma za TEHAMA mashuleni na katika vituo vya afya ambao unafanywa na watu pamoja na tasisi mbalimbali za umma na binafsi.

 

Aidha, Mkurugenzi wa Shule Direct, Faraja Kotta Nyalandu amesema kuwa wao kama wadau wa elimu wanashukuru Serikali kwa kuipa kipaumbele sekta ya elimu nchini kwa kuandaa mkakati wa kukuza na kuboresha matumizi ya TEHAMA shuleni ili wanafunzi na walimu waweze kufanya vizuri kwa maendeleo ya Taifa.