Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

DKT. CHAULA AZUNGUMZIA ELIMU YA AFYA YA UZAZI KWA MTOTO WA KIKE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula (katikati) akizungumza kabla ya kuzindua tovuti ya shirika lisilo la Serikali la Action Girls Foundation, jijini Dodoma. Kushoto ni Mkurugenzi wa Shirika hilo Rabia Saad akifuatiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Usalama Mtandao wa Wizara hiyo Eng. Steven Wangwe na wa pili kulia ni Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Lishe  wa TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe

 

 DODOMA

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amesema kuwa elimu ya afya ya uzazi kwa mtoto wa kike ni muhimu kwa sababu wanatakiwa kulindwa na kukingwa na changamoto zinazowakabili katika mazingira yao ya makuzi ili waweze kutimiza ndoto zao na jamii kwa ujumla

Dkt. Chaula ameyasema hayo wakati akizindua tovuti ya Shirika lisilo la Serikali la Action Girls Foundation jijini Dodoma leo tarehe 31.08.2021 ambapo alilipongeza Shirika hilo kwa kazi nzuri ya kuwajengea msingi bora watoto wa kike ili kuepukana na changamoto mbalimbali zinazokwamisha ndoto zao ikiwemo mimba za utotoni

“Nimefurahishwa na shughuli zinazofanywa na Shirika hili za kulinda ndoto za mtoto wa kike kwasababu wanawake wengi waliofanikiwa ndoto zao pia zililindwa na watu wengine”, alizungumza Dkt. Chaula

Amesema kuwa mashirika yasiyo ya Kiserikali ni sehemu ya mafanikio ya Serikali ndio maana kuna Sheria ya Public Private Parternership (PPP), hivyo mashirika haya pamoja na asasi za kiraia kwa kushirikiana na Serikali yanafanya kazi kubwa ya kutoa elimu ya afya ya uzazi na haki za mtoto wa kike ili kuwajengea uwezo wa kujitambua na kutimiza ndoto zao

Dkt. Chaula amezungumzia msingi wa msichana bora unaanzia katika makuzi kulingana na jamii inayomzunguka na Serikali inatoa chachu ya mafanikio kwa kutengeneza Sera kanuni taratibu sheria na miongozo zinazoelekeza ni namna gani ya kumlinda msichana huyu dhidi ya mazingira hatarishi ambayo yanaweza kuzima ndoto za mtoto wa kike

Ameongeza kuwa ili kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato na mtoto wa kike ana nguvu ya kujenga au kubomoa taswira yake kwa muonekano, mazungumzo na matendo yake mwenyewe

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Afya na Lishe wa TAMISEMI, Dkt. Ntuli Kapologwe  ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi ya Shirika hilo amesema kuwa Shirika hilo ni wadau wakubwa wa Serikali katika kuhakikisha wanapambana na mimba za utotoni na kumfanya mtoto wa kike ajitambue na kuweza kujali thamani yake kuwa na mchango wao kwa Taifa

Amesema kuwa taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI pamoja na  Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika kuhakikisha kuwa wanaweza kuinua thamani ya mtoto wa kike na kusaidia mapambano dhidi ya changamoto zinazomkabili mtoto wa kike

Amesema kuwa Serikali pekee haiwezi kuyafikia maeneo yote bila ushiriki wa asasi za kiraia na taasisi zisizo za Serikali ambapo kwa upande wa Serikali inatoa ushirikiano wa kutosha ili kufikia malengo yaliyowekwa ya kitaifa na kimataifa

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Action Girls Foundation, Bi Rabia Saad amezungumzia shirika hilo kuwa linafanya kazi ya kukuza uelewa wa wasichana juu ya afya ya uzazi na haki ambapo programu zao zinawafikia wasichana walio ndani na nje ya shule kwa kukuza uelewa wao juu ya afya ya uzazi, jinsia na hedhi salama kwa kutoa taulo za kike kwa wanafunzi wenye uhitaji.

Ameongeza kuwa hadi sasa Shirika hilo limeshawafikia zaidi ya vijana 1500 kupitia klabu za afya za shule za sekondari katika wilaya ya Mpwapwa Mkoani Dodoma na uwajengea uwezo wanafunzi, walimu walezi wa klabu, wazazi na kushirikisha watoa huduma za afya katika kufikisha elimu ya afya ya uzazi kwa vijana hao.

Mkurugenzi huyo ameseme kuwa katika kipindi cha miaka 2 ya Shirika hilo limeshirikisha waelimishaji rika takriban 300 nje ya shule, ambao wamefundishwa juu ya VVU / UKIMWI na hatua za kuzuia ukatili wa kijinsia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali pamoja na Wizara ya Afya ambapo kampeni za uhamasishaji walizozifanya zimefikia zaidi ya watu 500,000 katika mkoa wa Dodoma kupitia vipindi vya redio za hapa.