Tanzania emblem
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

Habari

BARAZA LA MAWAZIRI LIMERIDHIA UTUNGWAJI WA SHERIA YA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI AMBAYO ITAONGEZA USALAMA WA ANGA YA MTANDAO WA TANZANIA NA WANANCHI WAKE


Na Chedaiwa Msuya,WHMTH,  DAR ES SALAAM.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Nape Nauye (Mb) amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Habari, itahakikisha inaweka nguvu kubwa ili kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa kidijitali Afrika Mashariki kufuatia uwekezaji mkubwa unaofanywa kupitia sera na mipango mbalimbali ya kimaendeleo.

Waziri Nape ameyasema hayo Septemba 7, 2022 katika kongamano la siku mbili la kuunganisha wadau wa TEHAMA na Miundombinu (Connect 2 Connect) ndani na nje ya Tanzania katika Ukumbi mikutano Serena Hotel jijini Dar es Salaam na kusema kuwa, serikali itamuunganisha kila mwananchi kutumia baraka ya Teknolojia ya Mawasiliano na kubadilisha maisha ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

“Uwepo wenu hapa unaiweka Tanzania kwenye ramani nzuri kwa kuonesha hatupo tayari kumuacha hata mtu mmoja nyuma, lakini kwa niaba ya serikali niwahakikishie kuwa tutamuunganisha kila mmoja kutumia baraka ya teknolojia na mendeleo yake, na baraza la mawaziri limeruhusu kutungwa sheria itakayolinda taarifa binafsi na tunataka anga la mtandao wa Tanzania liwe salama kwa kutunga sheria bora” amesema. 

Amesema Serikali imepokea maoni ya wananchi na wadau wote waliopendekeza mabadiliko katika sekta ya mawasiliano nchini na hivyo kwenda kusomwa katika kikao cha Bunge tarehe 13 Septemba 2022 na pindi sheria hiyo ikipitishwa kutatungwa sheria bora ya kulinda taarifa binafsi kwa kila mtanzania.

Amesema, serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, unajitahidi kwa kiasi kikubwa kukuza maendeleo ya kidijitali kuendana na mapinduzi ya nne ya viwanda duniani, na serikali imewekeza miundombinu rafiki kuhakikisha kila mtanzania anapata huduma ya mtandao.

Amesema, ili kuhakikisha matumizi mazuri ya mtandao na teknolojia, serikali itahakikisha maadili ya utumiaji wa mtandao ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho kwa kufikisha elimu kwa vijana kutumia fursa mbalimbli zilizopo mitandaoni kujiinua kiuchumi, na kuwakaribisha wadau mbalimbali kuweka nguvu zaidi katika ukuaji wa teknolojia na mawasiliano nchini.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni binafsi inayojenga minara na inayofanyakazi na kampuni zote za mawasiliano nchini Helios Tower Tanzania (HTI) Bwn Gwakisa Stadi amesema HTT imedhamiria kuwa mstari wa mbele katika urahisishaji na ukuaji wa mawasiliano simu barani Afrika na Mashariki ya Kati, ikitambua umuhimu mkubwa wa uungwanishwaji Pamoja na manufaa yake kwa Watanzania na HTT inajivunia kuwa mmoja wa mfadhili wa Conect 2 Connect Summit.

Kwa upande wake Bwan Tariq H Malik, Mkurugenzi wa kampuni ya Extensia Tanzania amesema kutokana na umuhimu wa Mawasiliano na Teknolojia katika Nyanja mbalimbali za kimaendeleo kama biashara, elimu, sayansi na afya, watahakikisha wanashirikiana na serikali kuwa na miundombinu rafiki kwa ajili kizazi kijacho, na kuwapongeza wadau mbalimbali wa sekta ya mawasiliano ikiwemo TTCL kwa kufikisha mawasiliano Mlima Kilimanjaro pamoja na kampuni ya Vodacom kwa kuwa kampuni ya kwanza Tanzania kuleta huduma Yenye kasi ya 5G na kupitia mifano hiyo, sekta ya mawasiliano nchini inakua kwa kasi zaidi.